Ni miaka mitatu sasa tangu kufariki kwa Steven Kanumba, mmoja kati ya waigizaji mahiri waliojipatia mamia ya mashabiki kutokana na kazi zake nzuri. Kwa watu wake wa karibu, na pengine mashabiki wote, kifo chake kilikuwa ni cha ghafla na cha kushtua sana.
Kwa tuliomfahamu kiasi, huu siyo tena wakati wa kurejea maisha yake, kwa sababu tulijua nini alitaka katika maisha yake ya uigizaji na kwa kiwango kikubwa, alielekea kufanikiwa kulitangaza jina lake na nchi kwa jumla katika uso wa kimataifa.
Hadi hapo sheria itakavyosema vinginevyo, tunaendelea kuamini kuwa kifo chake kilikuwa ni makusudi ya Mwenyezi Mungu, kwamba kila nafsi itaonja mauti, iwe kwa namna ambayo binadamu wataridhika au la. Wakati akifariki dunia, usiku ule wa Aprili 6, 2012, Kanumba alikuwa chumbani na mpenzi wake, Elizabeth Michael ambaye wengi tunamfahamu zaidi kama Lulu.
Lulu alikuwa bado binti mdogo wakati huo, kiasi kwamba hata baada ya mamlaka kumkamata na kumuweka korokoroni, makundi mengi ya kijamii yalimuonea huruma na haikushangaza alipotolewa rumande kwa dhamana. Ni kweli alikuwa naye chumbani, ni kweli kulikuwa na mgogoro wa kimapenzi baina yao na ni kweli pia kwamba alimuona Kanumba akianguka.
Lakini hatuwezi kumhukumu, kwa kuwa kesi ipo mahakamani, tusubiri maana tunaamini haki itatendeka.
Baada ya kifo chake, mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa amejitokeza na kuwa ndiye mrithi wake. Ninajua mama huyu ndiye anahusika na vitu vingi vya marehemu, zikiwemo mali zake.
Kwa kutambua kwamba kazi ya Mungu haina makosa, tangu mwanzo wa msiba, mama Kanumba aliweka wazi kuwa hawezi kumhukumu Lulu, atampenda kama mkwe wake kwa kuamini kuwa mwanaye alimpenda. Tumeshuhudia, familia hizi mbili, ya Mama Kanumba na Mama Lulu wakiwa karibu zaidi kiuhusiano kuliko wakati marehemu akiwa hai.
Binafsi, nimeshawahi kukutana nao, siyo mara moja au mbili, wazazi hawa wawili wakiwa pamoja. Ni marafiki. Na mara kadhaa pia, Lulu ameonekana akiwa pamoja na mama wa mpenzi wake, akisema wazi kuwa atamchukulia kama mzazi wake.
Kijuujuu, tunatambua kuwa maisha yanaenda sawa kati ya familia hizo, wakiishi kama ndugu na kwamba kifo cha Kanumba hakijaleta uhasama, jambo ambalo ndilo muhimu zaidi.Lakini
kauli ya mama Kanumba hivi karibuni, aliyeongea kwa masikitiko juu ya kutupwa na Lulu, inapaswa kujadiliwa. Kwangu mimi nadhani umma unapaswa kumsaidia mama huyu ili kumweka sawa kisaikolojia, maana atakuwa na amani zaidi kuliko anavyoishi hivi sasa.
Sielewi anaposema Lulu amemtupa anamaanisha kutupwa kivipi, lakini kwa namna walivyokuwa wakiishi, ni rahisi kwangu kujua kuwa analalamika kwa vile binti huyo hivi sasa hamjali kama zamani alipomchukulia kuwa sawa na mama yake mzazi. Alijitahidi kugawana naye chochote kidogo alichopata.
Nimkumbushe tu mama kuwa siku zote, hisani zina mwisho. Na hata akigeuka nyuma na kuangalia maisha baada ya mwanaye kufariki, atagundua kuwa alipata misaada mingi mwanzoni, lakini kadiri siku zilivyokwenda, ikapungua. Hii ndiyo ‘nature’ ya binadamu.
Kama Lulu alikuwa karibu naye wakati ule, ni kwamba alitimiza wajibu wake, kwanza kama mpenzi wa mwisho wa mwanaye na pili kama mtu anayehusishwa na kifo hicho. Kibinadamu, alipaswa kufanya kama alivyofanya. Lakini kutaka Lulu aendelee kuwa karibu, ni sawa na kumtaka awe mtumwa.
Yule binti anahitaji maisha yake, yeye na familia yake. Litakuwa jambo la ajabu sana kama mama Kanumba atategemea maisha yake kuendeshwa na Lulu. Alijitahidi kadiri alivyoweza na kwa mtu mwenye busara, alipaswa kumshukuru kuliko kumshutumu.
Ni vyema kumuacha huyu mtoto aendelee na maisha yake, ana watu wengi nyuma yake. Ni dhambi, kumlaumu Lulu kwa maisha yoyote anayoishi mama Kanumba kwa sasa, hizi ni changamoto ambazo Mungu aliamua kumuachia huyu mama, azikabili!
Loading...
Post a Comment