MWANANCHI
Kwa mara nyingine, Jina la nchi limeendelea kuchafuka baada ya Meli ya MV Hamal iliyosajiliwa Tanzania kukamatwa Ulaya ikiwa imebeba shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine yenye uzito wa tani tatu, kama dawa hizo zingeuzwa mitaani nchini Uingereza zingekuwa na thamani ya Sh1.5 trilioni, kiasi ambacho nchi wafadhili zinatarajiwa kuichangia Tanzania kwenye bajeti ya mwaka 2015/16.
Mwaka 2013 meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa Tanzania ambayo ilikamatwa Septemba 2013 katika bahari ya Mediterranian, Italia wakati ikielekea Uturuki ikiwa na tani 30 za bangi zenye thamani ya Pauni 50 milioni za Uingereza (sawa na Sh125 bilioni).
Kiwango hicho cha dawa zilizokamatwa kimeweka rekodi ya ukubwa wa mzigo wa dawa hizo haramu zilizowahi kukamatwa Uingereza..
“Upekuzi wa meli ulikuwa mrefu na unaosababisha maumivu, na uliofanywa na watu wenye utalaamu mkubwa wa kufanya kazi kwenye mazingira magumu”—alisema John McGowan, afisa mwandamizi wa Uchunguzi wa NCA.
Rekodi za mtandao wa shughuli za baharini unaonyesha kuwa katikati ya Februari, meli hiyo ilikuwa Uturuki na wiki mbili zilizopita ilianza safari kutoka visiwa vya Tenerife, Hispania.. ilipokamatwa ilikuwa inaelekea Hamburg, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ujerumani ambako ingefika jana usiku.
Meli hiyo imekutwa na watu tisa wenye umri kati ya miaka 26 na 63 wote raia wa Uturuki na wameshitakiwa kwa kukutwa na dawa za kulevya.
JAMBO LEO
Chama cha Wamiliki wa Mabasi TABOA kimesema uwepo wa mizani ya kupima mizigo ya Kibaha imekuwa sababu mojawapo kubwa ya madereva kwenda mwendokasi ili kufidia muda mwingi ambao wanaupoteza kwenye mizani hiyo.
“Hii mizani mpya imekuwa ni tatizo kwetu, imekuwa ikichangia dereva kuendesha mwendo mkali kwani katika kupima mizani pale unachukua muda mrefu kukaa”—Enea Mrutu, Katibu Mkuu TABOA.
Alisema kwamba katika Kamati ambayo waliunda kuchunguza tatizo hilo la ajali wamegundua kwamba mwendo kasi pamoja na mizani hiyo vimechangia tatizo la ajali.
JAMBO LEO
Viongozi wa CHADEMA Rungwe, Mbeya wametwangana makonde mkutanoni baada ya kupishana kauli kwa kila mmoja kumpigia chapuo mtia nia ya Ubunge na kusababisha mmoja wao kuchanwa uso na kushonwa nyuzi sita.
Mwenyekiti wa Kitongoji ambaye alijeruhiwa amesema kisa cha ugomvi huo ni mgogoro wa maslahi binafsi anayoyaendekeza Katibu Uenezi wa Wilaya.
Kisa cha mgogoro wao ni suala la CHADEMA kupata nyumba ya kupanga ambayo wanaitumia kama ofisi, viongozi wote walichanga pesa kwa ajili ya ofisi hiyo lakini kiongozi mmoja ambaye ni Godogo aligoma akitaka ofisi hiyo ihamie nyumbani kwake kitu ambacho Kamati ilikataa.
Katibu wa Chama hicho Wilaya hiyo, Nsajigwa Bonifas amekiri kutokea tukio hilo na kusema ni kitendo cha aibu japo haweza kuzungumzia zaidi kwa sasa.
HABARI LEO
Wakati wateja wa umeme wameendelea kutaabika, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limetoa malekezo zaidi ya namna ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi.
Taarifa ya Tanesco imekuja baada ya tatizo lililojitokeza kwa baadhi ya mawakala wa LUKU kushindwa kutoa huduma ya kuuza umeme kutokana na Kampuni ya SELCOM ambaye ni wakala wa kuuza na kuziunganisha baadhi ya kampuni za simu kwa TANESCo kusitishiwa huduma kutokana na kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yake ikiwamo kughushi nyaraka na kukiuka taratibu za kulipa kodi.
Taarifa iliyotolewa jana na shirika hilo, na kusainiwa na Ofisa Habari wake, Adrian Sevelin ilisema kuwa huduma zinaendelea kupatikana kupitia Makampuni mengine na huduma za Mabenki.
“Shirika linaomba radhi kwa usumbufu wowote unaojitokeza, wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa”– alisema Adrian Sevelin, Afisa Uhusiano wa TANESCo.
Gazeti la HABARI LEO lilizunguka katika vituo mbalimbali vya kutoa huduma hiyo na kukuta misululu ya wananchi wakisubiri huduma hiyo huku kukiwa na tatizo la mtandao.
MTANZANIA
Mwenendo wa uchunguzi wa madai ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa kutaka kuuawa na mlinzi wake binafsi, Khalid Kangezi, umezua shaka kutokana na ukimya wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ambapo kwa zaidi ya mwezi mmoja limeshindwa kuwahoji watuhumiwa waliotajwa.
Uchunguzi wa gazeti la MTANZANIA umebaini Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana ambao kwa pamoja wanashutumiwa kula njama ya kutaka kumzuru Dk. Slaa,hawajahojiwa.
“Si Mangula wala Kinana aliyehojiwa.. inasikitisha kuona watu walioendesha njama ya kutaka kuteketeza maisha yangu wanaendelea kuranda randa pasipo hatua yoyote kuchukuliwa,” alisema Dk. Slaa.
Alipotafutwa Philip Mangula ili athibitishe kama ameshahojiwa na Jeshi la Polisi au la, alishindwa kukataa wala kukubali badala yake alimwambia mwandishi kuwa yupo kwenye kikao na hata alipotafutwa Kinana simu yake haikupatikana.
“Ngoja niulize wasaidizi wangu…Lakini kwanini umeniuliza swali hilo wakati sipo ofisini? Nitafute Jumatatu,” alijibu Kamishna Kova baada ya kuulizwa kuhusu suala hilo
Post a Comment