Mamia ya wanachama na mashabiki wa Chadema jana walifika katika ofisi
za Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni Dar es Salaam kumsubiri Katibu
Mkuu, Dk Willbrod Slaa baada ya kuenea habari kuwa angeingia ofisini.
Hata hivyo,wanachama hao waliokuwa na shauku ya kumwona kiongozi huyo,
hawakufanikiwa baada ya kuambiwa kuwa Dk Slaa asingefika katika ofisi
hizo kinyume na taarifa zilizokuwa zimetolewa kuhusu kurejea kwake.
Juzi mzee Philemon Ndesamburo na makada wengine wa chama walikwenda
nyumbani kwa Dk. Slaa kwa ajili ya mazungumzo, na kwamba alikubali
akasema angerejea ofisini jana
Kwa muda mrefu Dk Slaa hakuonekana kwenye matukio muhimu ya Chadema na
yale ya Ukawa, kama wakati wa kumkaribisha Edward Lowassa ndani ya chama
hicho, wakati Lowassa alipochukua kadi na alipochukua fomu ya kuwania
urais.
Kadhalika kiongozi huyo hakuonekana katika Baraza Kuu la Chadema,
mkutano wa Kamati Kuu na Mkutano Mkuu uliompitisha kwa kauli moja kuwa
Lowassa aipeperushe bendera ya urais chini ya mwamvuli wa Ukawa.
Akihutubia Baraza Kuu la chama hicho wiki iliyopita, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa chama kiliridhia Dk Slaa apumzike
wakati mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu ukiendelea baada ya Katibu
Mkuu huyo kutofautiana katika uamuzi wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa.
Baraza Kuu lilipiga kura ya wazi na kushauri kuwa endapo atafikiria
kubadili uamuzi wake, anaweza kuendelea na harakati za chama hicho
kuelekea Ikulu chini ya muungano wa Ukawa.
Mwandishi wetu aliyefika katika ofisi za Chadema zilizopo katika Mtaa wa
Ufipa, Wilaya ya Kinondoni, alishuhudia idadi kubwa ya wanachama wakiwa
wamekusanyika katika vikundi wakijadili masuala mbalimbali huku
wakimsubiri Dk Slaa.
“Nimesikia taarifa kuwa kuna watu hapa wanamsubiri Dk Slaa nikaja
kushuhudia, watu wanaongea mambo mengi kama vile Ukawa imevunjika wakati
kila kitu kinakwenda sawa hapa,” alisema Ali Mundu mmoja wa wananchama
hao.
Loading...
Post a Comment