Jeshi la Polisi nchini linafanya uchunguzi kumbaini mmiliki wa ukurasa
wa twitter unaoendeshwa na anayejiita Daudi Balali, aliyewahi kuwa
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili hatua za kisheria zichukuliwe
dhidi yake.
Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba,
aliyasema hayo wakati akizungumza na Gazeti la Nipashe ofisini kwake
jana.
Bulimba alisema kuwa taarifa za uwapo wa ukurasa huo wa twitter,
wamekwishazipata na wanafanya uchunguzi wa kina kumkamata mhusika kisha
kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Tunazo taarifa juu ya ukurasa huo wenye wafuasi wengi kwa sasa na
unaotumika kuwashambulia viongozi wa serikali na wa siasa hasa wale
wanaogombea nafasi kubwa za utawala nchini, hivyo Jeshi la Polisi lipo
kwenye uchunguzi ili kumbaini mtu huyo haraka iwezekanavyo,” alisisitiza
Senso.
Ukurasa huo ulioanza kutumika kabla ya Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni
kuanza kutumika, una wafuasi zaidi ya 6,000 kwa sasa na umekuwa
ukitumika kuwachafua wagombea urais nchini hasa wa upinzani.
Aidha, umekuwa ukitabiri matokeo ya uchaguzi, kitendo ambacho kimekuwa kikiwachanganya wananchi.
Bulimba alisisitiza kuwa jeshi hilo liko makini na linafuatilia hivyo mtu huyo atasakwa na kukamatwa akiwa mahali popote.
Aliwataka pia wananchi kuripoti katika vituo vya polisi pindi wanapopata
vitisho vya aina yoyote, kudhalilishwa ama kufanyiwa kitu chochote
kibaya kupitia mitandao ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
“Jeshi la polisi linafanya kazi usiku na mchana, hivyo mtu yeyote
asijidanganye kwamba atavunja sheria na asikamatwe, maana tuna njia
nyingi za kuwabaini watu hao kwa kushirikiana vyema na TCRA pamoja na
wananchi, hivyo chanzo chochote kinachohusu uhalifu wa mtandaoni,
kitashughulikiwa,” aliongeza.
Aliwaonya pia watu waliokuwa wakitumia kurasa mbalimbali kwenye mitandao
ya kijamii kwa kutumia majina ya watu wengine ili kudhalilisha watu na
kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo juu ya masuala mbalimbali
kuachana mara moja na tabia hiyo maana wakibainika watachukuliwa hatua
kali za kisheria na kuwa mfano kwa wengine wanaojihusisha na vitendo
hivyo.
Loading...
Post a Comment