USHIRIKI wa waziri mkuu wa zamani,
Edward Lowassa katika vita vya kumng’oa Nduli Idd Amin wa Uganda mwaka
1978/79 umeibua gumzo kufuatia madai ya katibu mkuu wa zamani wa CCM,
Yussuf Makamba kushabihiana na ya Makongoro Nyerere aliyedai kuwa
hakuwahi kumwona mstari wa mbele.
Rais wa awamu ya kwanza wa Tanzania, Mwl. J.K Nyerere na makamanda wa Jeshi.
Katika mkutano wa kumnadi mgombea wa
chama chake, Makamba alidai kuwa anashangazwa na madai ya Lowassa kuwa
alikwenda vitani, wakati aliyeandikisha majina ya askari waliokwenda
huko wakati huo alikuwa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye hakuwahi
kuorodhesha jina hilo.
Wakizungumzia suala hilo, watu
mbalimbali waliopiga simu chumba chetu cha habari, walisema ni vyema
kama Lowassa angejitokeza na kuthibitisha madai hayo, kwani akikaa
kimya, ataonekana ni mwongo, kitu ambacho ni kibaya kwa kiongozi
anayeomba kuwa rais wa nchi.
“Maneno kama haya niliwahi kumsikia
akiyasema Makongoro, kwamba hakuwahi kumuona Lowassa mstari wa mbele,
leo Makamba anasema jina lake halikuandikwa na Kikwete, ni vizuri
akajitokeza ili athibitishe kama kweli alienda au la!” alisema Shauri
Shamim, aliyedai kupiga simu akitokea Tanga.
“Hili ni jambo kubwa, siyo dogo kama
inavyoweza kudhaniwa, tunajua kuwa Lowassa aliwahi kuwa askari,
ajitokeze na kuzijibu tuhuma hizi za wanajeshi wenzake ili tujue kama ni
propaganda za kisiasa au la!” alisema Jane Jarome wa Masasi.
Mei mwaka huu, wakati wa mkutano wake na
wahariri wa vyombo vya habari mjini Dodoma, pamoja na mambo mengine,
Lowassa alisema alikuwa miongoni mwa askari wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) walioshiriki vita vya kumng’oa madarakani kiongozi huyo
wa Uganda aliyeivamia Tanzania.
Post a Comment