Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ameponda
kauli ya vyama vya upinzani kuwa vitaleta mabadiliko, akisema kazi hiyo
tayari imefanywa na CCM.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Uhuru mjini
Bukoba wakati wa uzinduzi wa kampeini za wagombea wa chama hicho mkoani
Kagera, Mkapa alisema chama pekee kilichobobea katika ukombozi ni CCM
na Serikali zake zilizotangulia.
Kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya
Tatu alisema kuwa lengo la vyama vya upinzani ni kuing’oa CCM na lengo
la chama hicho tawala ni kuendelea kushika dola, hivyo upinzani
unatakiwa kujifunza hadi baada ya miaka 50.
Alitaja miradi mbalimbali ya maendeleo
iliyotekelezwa kwa awamu tofauti kuwa ndiyo aina ya mabadiliko ya
maendeleo wanayohitaji wananchi, akitaja uwanja wa ndege wa Bukoba na
barabara za lami.
“Hayo ndiyo mabadiliko ya maisha ya
Watanzania huwezi kuleta ajira kwa kutamka tu, tulianzisha wilaya na
mikoa mipya ili kuchochea maendeleo ya wananchi na maisha yao hayo ndiyo
mabadiliko,’’ alisema Mkapa.
Jana, alionekana kuzungumza kwa tahadhari kwa kile alichodai akiwaeleza wapinzani ukweli wanadai ana jeuri.
Hata hivyo, katika hotuba yake alishindwa kujizuia na kutamka neno mbumbumbu na kusema hataki kuwazungumzia.
Kabla ya kumkaribisha Mkapa kuhutubia,
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye alisema wagombea wote
wamepita kwenye mchujo sahihi na kutamba kwamba chama hicho kimejipanga
kupata ushindi.
Post a Comment