Polisi mkoa wa Mara inamshikilia mwananke mmoja (jina tunalo) mkazi wa
Bweri Manispaa ya Musoma kwa kosa la kumchoma mtoto wake mwenye miaka
minne, kwa maji ya moto, mikono yote miwili baada ya kumtuhumu kuwa
ameiba nyama jikoni.
Mama huyo alikamatwa Novemba 14 saa nne asubuhi katika eneo la Morembe
kata ya Bweri mjini Musoma baada ya Polisi kufika nyumbani kwake
kumkamata kwa kosa jingine la kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali
za mwili Kabula Rubeni (32) akimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na
mume wake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, ACP Alex Philip Kallangi alidai kuwa
siku ya tukio hilo la kumchoma moto mtoto huyo, mama yake mzazi alikuwa
amepika nyama jikoni na baadaye alikwenda kuchota maji.
Kamanda Kallangi alidai baada ya mama huyo kurudi alimkuta mwanaye
anakula nyama ndipo alishikwa na hasira na kuanza kumchapa sehemu
mbalimbali za mwili wake na kisha akachukua mikono yote miwili na
kumchoma kwa maji ya moto.
Baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama, mama huyo alianza kumtibu
mtoto huyo kwa siri hapo nyumbani kwa dawa za kienyeji bila majirani
kufahamu kilichokuwa kikiendelea nyumbani kwa mama huyo.
Kamanda Kallangi alieleza kuwa kilichosababisha kufahamika kwa taarifa
hizo, ni baada ya Kabula aliyekuwa ameshambuliwa kwa mapanga na mwanamke
huyo kwenda polisi kutoa taarifa ya kushambuliwa.
Kallangi alieleza kwamba polisi walipofika nyumbani kwake ndipo walipewa
taarifa za mtoto huyo kujeruhiwa kwa kuchomwa moto. Kutokana na tukio
hilo polisi hao, kwa kushirikiana na maofisa ustawi wa jamii na kituo
cha ushauri cha Jipe Moyo walimchukua mtoto huyo na kumpeleka katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwa matibabu na kisha kupelekwa Jipe
Moyo anakoishi hadi sasa kwa uangalizi zaidi.
Kallangi alisema mtuhumiwa huyo yupo kituoni na anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu mashtaka yanayomkabili.
Ofisa Ustawi wa Jamii Musoma, Vedastus George aliwataka wazazi na walezi
kuzuia hasira zao pale watoto wanapowakosea na hata wanapowaadhibu wawe
makini ili waziwaumize kama alivyofanyiwa mtoto huyo.
Loading...
Post a Comment